KATIBU Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Dk. Willibrod Slaa, amemshambulia Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Abdulrahman Kinana, kwamba anashabikia mfumo wa serikali mbili ili anufaike na mfumo wa ufisadi na wizi wa rasilimali za Watanzania.
Dk. Slaa, alitoa kauli hiyo katika mkutano wa hadhara uliofanyika katika viwanja vya Mgereza mjini Geita, wakati akifafanua hoja mbalimbali zilizowafanya wajumbe wa Bunge Maalumula Katiba wanaounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (UKAWA), kususia vikao vyake.
Alisema Kinana, anapigana kufa na kupona akitetea serikali mbili kwa sababu zinaruhusu mafisadi waendelee kuiba mali za Watanzania bila kuwajibishwa na mamlaka zilizopo.
Slaa, alisema Kinana ni mmoja wa viongozi ambao kama kungekuwa na katiba bora angeshakamatwa na kushitakiwa kwa kuwa meli anayoimiliki ilikamatwa baharini ikiwa na nyara za taifa zenye thamani ya sh bilioni 5 ikielekea Hong Kong, lakini hadi leo hajachukuliwa hatua yoyote.
“Ndugu zangu mfumo wa serikali tatu unazuia ufisadi wa rasiimali za wananchi zisiibwe na kuchezewa na mafisadi, na ndiyo maana CCM na Kinana wanazunguka nchi nzima wakihubiri serikali mbili ili waendelee kupata mianya ya kuiba tembo na madini yetu bila kuchukuliwa hatua,” alisema.
Alisema Kinana amekuwa akiwadanganya Watanzania kuwa katiba mpya sio muarobaini wa matatizo yao, huku akijua fika kwamba haki za wananchi zinapati kana kwenye katiba yenyewe.
“Kinana amekuwa akipotosha Watanzania, anawaambia eti katiba mpya sio muarobaini wa matatizo yao, lakini anawadanganya, ni muongo, ni mnafiki wa hatari sana na vitabu vitakatifu vinasema yeyote anayepotosha walio wadogo anastahili kufungiwa jiwe shingoni na kutupwa baharini.
“Haki zote za msingi za binadamu zinazomlinda na kumtetea mwananchi wa kawaida lazima zipatikane kwenye katiba na ziwekewe masharti ya kuziheshimu ili zitendeke, na ndiyo maana Afrika Kusini mwaka jana wananchi walipeleka kesi mahakamani na imeruhusiwa mwananchi wa Afrika Kusini asipotibiwa anashitaki serikali, lakini kwa Tanzania usipopata maji, elimu au matibabu huwezi kuishtaki serikali,” alisema Dk. Slaa.
Mkutano huo ulihutubiwa pia na viongozi wengine wa UKAWA kutoka Chama cha Wananchi (CUF) na NCCR-Mageuzi.

No comments:
Post a Comment