Wanafunzi wa shule ya sekondari kiteto wakionyesha vitabu baada ya kukabithiwa na kampuni ya simu za mkononi ya Airtel chini ya mradi wake wa Airtel shule yetu wenye lengo la kuchangia katika sekta ya elimu nchini.
Na Mwandishi wetu
Kampuni ya simu za mkononi ya Airtel imepiga jeki jitihada za serikali za kuhamasisha masomo ya sayansi kwa kutoa msaada wa vitabu vya sayansi kwa shule ya sekondari ya Kiteto iliyopo mkoani Manyara.
Msaada huo wenye thamani ya shilingi milioni 1.5 unahusisha vitabu vya fizikia, hisabati, baiolojia na kemia kwa ajili ya wanafunzi wanaosoma masomo hayo katika shuleni hiyo.
Akipokea msaada huo Diwani wa kata ya Central wilayani Kiteto Mh Yahya Masumbuko, amesema shule nyingi wilayani hapo zimekuwa zikikabiliwa na changamoto ya upungufu wa vitabu vya masomo ya sayansi licha ya kwamba kuna uhaba pia wa walimu wa masomo hayo.
“Ni kweli kwamba uhaba wa vitabu unakwamisha kwa kiasi kikubwa wanafunzi kujifunza kwa ufasaha masomo ya Sayansi wilayani Kiteto hali inayorudisha nyuma ukuaji wa elimu ya sayansi wilayani hapa”. Alisema Mh Masumbuko.
“Uhaba wa vitabu ni moja ya changamoto, lakini uhaba wa walimu wa masomo ya sayansi pia ni kikwazo kikubwa kwa utoaji wa elimu ya sayansi kwa wanafunzi wetu hapa wilayani” aliongeza Mh Masumbuko.
Aidha Diwani huyo ameishukuru kampuni ya simu ya Airtel kwa kuona umuhimu wa kuboresha masomo ya sayansi ambayo ufaulu wake umekuwa mdogo hali ambayo inayotoa fursa kwa wanafunzi kujifunza kwa umakini zaidi.
“Msaada huu utaongeza hamasa kwa wanafunzi wetu kujifunza masomo ya sayansi hivyo tunawashukuru sana Airtel kwa kuona umuhimu wa kusaidia shule hii na hasa vitabu vya sayansi” alieleza Mh Masumbuko.
“Sisi wa Kiteto tunaendelea na jitihada za kuhakikisha wanafunzi wetu wanajifunza masomo hayo na ndio maana hata mgao wa walimu tulioupata tumeuelekeza katika ufundishaji wa masomo ya Sayansi. Alimalizia Mh Masumbuko.
Kwa upande wao baadhi ya wanafunzi wa shule ya sekondari Kiteto wameishukuru kampuni ya simu za mkononi ya Airtel kwa kuwawezesha kupata vitabu vitakavyowasaidia katika masomo yao.
Msaada huo wa vitabu vya masomo ya hisabati,kemia,fizikia na Bailojia utasaidia kupunguza uhaba wa vitabu vya sayansi kwenye shule hiyo ya wilayani Kiteto mkoani Manyara.
Airtel shule yetu ni mpango endelevu uliodumu kwa takribani miaka 10 iliyopita mpaka sasa zaidi ya shule za sekondari 1300 nchini zimeidika na msaada wa vitabu chini ya mradi huu.
Tutaendelea kushirikiana na serikali chini ya wizara ya elimu katika kuhakikisha tunaboresha sekta ya elimu na kutoa kipaombele kwenye masomo ya sayansi ili kuwa na wanasayansi wengi nchi ambao kwa sasa ni changamoto katika shule nyingi na nchi kwa ujumla alisema Meneja mauzo wa Airtel kanda ya kati Bwana Hendrick Bruno
Toa Maoni Yako:
0 comments: