Hawa Kundani (mwenye vazi jeusi), anayedai kuzaa na kutelekelezwa na mbunge wa Dimani, Abdallah Sharia Ameir, akiwa chini ya ulinzi wa polisi baada ya kuvamia kikao cha Kamati ya Bunge ya Katiba, Sheria na Utawala kilichokuwa kikifanyika Dar es Salaam jana. Picha na Beatrice Moses .

Na Mwandishi Wetu.

Mwanamke aliyetambulika kwa jina la Hawa Kundani amezua taharuki kwenye kikao cha Kamati ya Bunge ya Katiba, Sheria na Utawala, baada ya kuvamia ghafla na kupiga kelele akidai kutelekezwa na mumewe ambaye ni Mbunge wa Dimani (CCM) visiwani Zanzibar, Abdallah Sharia Ameir.

Tukio hilo la aina yake lilitokea jana kwenye Ukumbi wa Mikutano wa Kimataifa wa Mwalimu Nyerere, na mwanamke huyo akiwa ameongozana na mtangazaji wa kituo kimoja cha redio, Joyce Kiria aliingia na kusababisha mshtuko kwa wajumbe wa kamati hiyo na viongozi wa dini ya Kikristo waliokuwa wamealikwa hapo. Wakati huo walikuwa wakijadiliana suala la Mahakama ya Kadhi.

Hawa akizungumza na gazeti hili alidai kwamba Ameir ni mume wake walifunga ndoa mkoani Arusha mwaka 1999 na kuzaa naye watoto wanne, lakini mmoja alifariki dunia.

“ Nashangaa amebadilika ghafla amekuwa mtu wa kuoa wanawake na kuacha mara kwa mara, hadi sasa ameshaoa wanawake wanne na kuwaacha mimi nipo tu, alinioa bado mdogo,” alidai Hawa.

Alidai kuwa watoto wengine wawili, mkubwa ana miaka tisa na mwingine miaka sita walichukuliwa na mumewe huyo akawapeleka kulelewa na mwanamke aliyemuoa jambo ambalo alidai linamuuma.

“ Naumia wanangu sijui wanaishi vipi, huyu niliyembeba ni mlemavu, hamtaki amekuwa akininanga kwa maneno mengi sana, mimi nimetoka naye mbali nilibadili dini kwa ajili yake, leo hii ananitesa, hanitaki anipe haki yangu ili niishi mwenyewe,” alisema Hawa.

Kwa upande wa mbunge hiyo Ameir alidai kwamba kesi yao ipo kwenye Mahakama ya Kadhi, akidai kwamba mwanamke huyo amekuwa akimdhalilisha kwa kupitia mtoto huyo mlemavu ambaye alikiri ni mwanaye.

“ Huyu ni mwanangu sishindwi kumhudumia, lakini sitaki fedha ziende kwa huyu mwanamke atazitumia kwa mambo yake mengine, mimi nilimpeleka kwa mama yake mzazi akakae naye huko lakini yeye hataki,” alisema Mbunge Ameir.

Akizungumzia tukio hilo Makamu Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Gosbert Blandes alisema ni tukio ambalo limewafedhehesha kwa kuwa hawakulitarajia.

“Tulivamiwa na wanawake kama wanne na wanaume wawili nafikiri mmoja alikuwa ni mpiga picha, mwanamke mmoja akawa anapiga kelele, tulitaharuki kwa sababu maaskofu walikuwa wameanza kutoa maoni yao,” alisema.

Alisema kwamba waliomba msaada kwa maofisa usalama wa ukumbi na walifika na kuwachukua wahusika hao, kisha kuwapeleka polisi kwa hatua zaidi.
Kajunason Blog

Kajunason Blog

A Tanzanian blog operating since October 2007, covering Local News, Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers / viewers.

Toa Maoni Yako:

0 comments: