NA MWANDISHI WETU, DAR ES SALAAM

MSANII wa muziki wa mashairi, Said Machenje, amesema ameanza mazoezi rasmi kwa ajili ya kuhakikisha kuwa anakuwa mmoja wa wasanii watakaotoa burudani kali katika tamasha la NSSF Handeni Kwetu, linalotarajiwa kufanyika katika Desemba 13 mwaka huu, katika Uwanja wa Azimio, mjini Handeni, mkoani Tanga.

Machenje anayeshindana vilivyo na mkali wa muziki huo, Mrisho Mpoto alisema kuwa maandalizi yake yanakwenda sambamba na shauku ya kutembelea kwa mara ya pili wilayani Handeni.

Akizungumza jana jijini Dar es Salaam, Machenje alisema kwamba mwaka jana alipanda jukwaani kuimba kwa kushirikiana na kikundi cha Naukala Ndima, ila msimu huu amefanikiwa kupata mwaliko wake binafsi.

Mwimbaji huyo wa 'Kajenge kwa Mumeo' na 'Mila', alisema kwa kualikwa binafsi, kunamfanya apate hamu ya kujiandaa kwa ajili ya kufanya mambo makubwa zaidi ili kuonyesha umahiri wake katika tasnia ya muziki wa mashairi.

“Nashukuru Mungu kwa kupangwa kuwa mmoja wa wasanii watakaotoa burudani katika tamasha la NSSF Handeni Kwetu 2014, wilayani Handeni mkoani Tanga kwakuwa ni mwelekeo mzuri katika maisha yangu ya sanaa.

“Nafanya mazoezi makali kwa ajili ya kujiweka sawa ili nifanye shoo nzuri Desemba 13, katika Uwanja wa Azimio, ukizingatia kuwa nina uzoefu sasa na jukwaa la tamasha hili la aina yake,” alisema.

Wadhamini tamasha hilo ni Shirika la Mfuko wa Hifadhi ya Jamii (NSSF) pamoja na Phed Trans, SmartMind & Partners iliyopo chini ya Anesa Co. Ltd kwa kupitia kitabu cha ‘Ni Wakati wako wa kung’aa, Handeni Kwetu Foundation, Wait & Watch Film Company Ltd, Qs Mhonda J Apex Group of Companies Ltd na Skyblue Security and Risk Mgt Ltd na Michuzi Media Group.
Kajunason Blog

Kajunason Blog

A Tanzanian blog operating since October 2007, covering Local News, Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers / viewers.

Toa Maoni Yako:

0 comments: