Kikwete na mtangazaji wa Cloud FM Mbwiga MbwigukeRais Dkt. Jakaya Kikwete akipozi katika picha na Mbwiga wa Mbwiguke wa Clouds fm (kulia)

Na Maregesi Paul

SIKU moja nilikuwa katika mkutano wa Jukwaa la Wahariri ambao mgeni rasmi alikuwa Mwenyekiti wa Kampuni za IPP, Reginard Mengi.

Katika mazungumzo yake, Mengi aligusia historia ya maisha yake ambapo alisema alikulia katika familia masikini.

Kwa mujibu wa Mengi, nyumba aliyokulia ilikuwa na panya wengi pamoja na mende na kwamba kila walipokuwa wakilala usiku, wapita njia walikuwa wakiwaona kwa sababu nyumba ilikuwa imejaa matobo.

Pamoja na mazingira hayo, Mengi kwa sasa ni kati ya matajiri wakubwa wanaoheshimika ndani na nje ya nchi na suala la umasikini aliokulia, limebaki kuwa historia.

Hivyo hivyo, hata mimi niliyeandika makala haya, niliwahi kuvua dagaa na sangara kwa kutumia nyavu haramu ziitwazo makokoro. Lakini sasa mimi ni mhariri wa gazeti hili na suala la uvuvi, limebaki katika historia.

Wakati hayo yakitokea, katika Radio Clouds kuna watangazaji wengi wanaovuta masikio na hisia za wasikilizaji kutokana na lugha na vichekesho wanavyovitumia pindi wanapokuwa studio.
Miongoni mwao ni Said Seleman maarufu kwa jina la Mbwiga wa Mbwiguke.
EX6Mbwiga wa Mbwiguke (kuli) akipozi na Shaffih Dauda kwenye moja ya mechi iliyoihusisha timu ya mpira ya Clouds Media Group maarufu kama ‘The Dream Team’

Kama ilivyo kawaida kwa watu kuwa na historia tofauti tofauti kama nilivyoeleza hapo awali, wakati wa mahojiano maalum na MTANZANIA Jumatatu, Mbwiga anaeleza kwa kirefu ni wapi alikotokea hadi akawa mmoja wa watangazaji maarufu katika radio hiyo maarufu nchini.

“Kwanza nianze na maana ya jina Mbwiga. Mbwiga ni neno la kizaramo ambalo maana yake ni rafiki. Kwa hiyo mimi ni rafiki wa kila mmoja kwa sababu huwa napenda sana kuwachekesha watu.
“Lakini pia, maisha ni mzunguko na kamwe hakuna binadamu anayezaliwa na kujua maisha yake yatakuwaje kwa siku zijazo.

“Kwa maana hiyo, hiki nitakachokieleza ndivyo kilivyo kwa sababu hapa nilipo sikutarajia kama itatokea siku nikawa mmoja wa watu wanaoungwa mkono na mamilioni ya Watanzania.

“Kwanza kabisa niseme tu kwamba, mtu aliyenifikisha hapa ni mtangazaji mwenzangu aitwaye Shafii Dauda. Huyu ndiye aliyenileta Clouds baada ya kuniona naweza kuwa na mchango fulani fulani katika redio yetu hii.
“Sikumbuki ni mwaka gani, lakini nakumbuka ni kama miaka mitatu iliyopita, siku moja usiku nilikuwa pale Muhimbili Shule ya Msingi kwenye mazoezi ya mpira unaowahusisha wachezaji wakongwe kama akina Akida Makunda, Mohamed Binda, Idd Moshi, Ally Mayai, Crement Kahabuka, Dua Said na wengineo wengi .

“Siku hiyo nilikuwa sichezi bali nilikuwa shabiki tu nikiwashangilia wenzagu, kwa hiyo, mazoezi yalipomalizika, Shafii Dauda alikuja mahali nilipokuwa na akina Ally Mayai na alitukuta tunacheka,” anasema Mbwiga na kuongeza.

“Alipoona tunacheka, akauliza tunacheka nini, Ally Mayai akamwambia huyu jamaa anatuchekesha, hebu mchukue umtumie kwenye kipindi chako kile cha michezo cha saa tatu usiku atakusaidia sana,” anasema Mbwiga.

Kwa mujibu wa Mbwiga, Shafii alikubali na hapo ndipo ukawa mwanzo wa safari yake kujiunga na Radio Clouds.

Anasimulia kwamba, baada ya kukubaliwa, Shafii akawa anampigia simu ili aripoti matukio mbalimbali ya michezo na kwamba taarifa hizo alikuwa akiziripoti katika mazingira magumu.
“Wakati mwingine nilipokuwa nikiripoti, kuna wakati Shafii alikuwa akinipigia simu nikiwa kwenye daladala, kwa hiyo, nilikuwa nikilazimika kushuka ili nitafute sehemu nzuri iliyotulia ili nirekodi kipindi.
Mtangaaji wa Clouds Fm, Mbwiga wa Mbwiguke (kushoto) akipozi na shabiki wake Imani Ntila.

“Jambo la kuwaeleza wapenzi wa Radio Clouds ni kwamba, wakati ule nilipokuwa nikirekodi kipindi na Shafii, nilikuwa nikifanya kazi pale Uwanja wa Azamu kule Chamazi. Kule Azam nilikuwa nikisafisha uwanja kwa kuokota vyuma na chupa za maji zilizokuwa zikitupwa wakati wa ujenzi na zilizokuwa zikitupwa na wachezaji walipokuwa wakifanya mazoezi.

“Lakini kumbuka kwamba, pale Azam nilikwenda kuomba kazi za uselemala, nilipokosa hiyo kazi, nikaangukia katika kusafisha uwanja kama nilivyokwambia.

“Kwa maana hiyo, kuna wakati nilipokuwa nikitakiwa kurekodi kipindi na Shafii, nilikuwa nikijificha kwenye majukwaa chini kabisa kwa sababu kule pametulia kweli kweli.

“Nilipokuwa nikifanya hivyo, wenzagu niliokuwa nikifanya nao usafi walikuwa wakilalamika kweli kwa sababu waliamini nategea kazi, kumbe mwenzao nilikuwa naandaa maisha,” anafafanua Mbwiga.
Mbwiga Mbwiguke akiwatuliza wanachama wa Yanga waliojitokeza kwenye mkutano mkuu wa klabu hiyo mwaka huu.

Baada ya kufanya kazi hiyo kwa miezi kama mitatu hivi, anasema baadaye Shafii aliamua kumpeleka ofisini kwao Mikocheni Dar es Salaam ambako alianza kutangaza akiwa studio.
Alipofika ofisini hapo, anasema alikutana na mmiliki wa radio hiyo, Joseph Kusaga ambaye alisoma naye Shule ya Msingi Forodhani (zamani St Joseph).

“Siku moja baada ya kuanza kutangaza, ilifanyika sherehe ya wafanyakazi wote ambapo MC alinipa fursa ya kuzungumza. Hapo nilimshukuru bosi Kusaga kwa kumwambia amenipa nyavu badala ya samaki, hivyo ni wajibu wangu kuendelea kuvua,” anasema Mbwiga.

MAISHA YAKE KAZINI
Mbwiga anasema baada ya kuanza kazi rasmi, anasema alikutana na changamoto nyingi ambazo ni pamoja na kutakiwa kujua mambo mengi yanayotokea duniani.

Pia anasema kwa kiasi fulani amefanikiwa kufikia malengo kwa kuwa pamoja na kutangaza katika kipindi cha michezo cha saa tatu usiku, hivi sasa anashiriki katika kipindi cha Power Breakfast kinachorushwa kila siku asubuhi.

“Nashukuru kwa sababu sasa niko katika vipindi viwili, yaani kile cha usiku na cha asubuhi na nadhani wakubwa wangu wameniongezea majukumu baada ya kuona nina msaada fulani kiofisi.
“Jambo la kushangaza ni kwamba, wakati naanza kutangaza Power Breakfast, moyo uliuma sana, yaani niliogopa kwa sababu sikujua kama ningeweza kufanikiwa.

“Lakini Jerad Hando alinitoa hofu, akaniambia usiogope, hakuna kitu kipya, nikamuelewa na mwishowe nikawa nimefanikiwa,” anasema.
Mbwiga Mbwiguke (kulia) akiwa na mdau wa michezo

MAISHA YAKE KWA SASA
Mbwiga anasema kwa sasa anaonekana mtu wa maana mtaani kwake anaokoishi Magomeni Dar es Salaam na Tanzania kwa ujumla tofauti na alivyokuwa mwanzo.

“Maisha yangu yamebadilika sana mtaani kwetu na jambo jingine ninaloshukuru ni kwamba, nina marafiki wengi na nafahamika kila mahali.

“Yaani hata Rais Kikwete ananifahamu kwa jina kwa sababu mwaka jana nilifuturu naye Ikulu tukiwa naye meza moja.

“Hata hivi karibuni tulikutana naye kwenye tamasha la wasanii kule Dodoma na aliponiona, aliniita kwa jina akaniambia, Mbwiga hujambo, nilimjibu, sijambo mheshimiwa, msimu wa embe nyani hakondi, halafu akacheka,” anaeleza.

HISTORIA KIFAMILIA
Anasema yeye ni mtoto wa pili kuzaliwa katika familia yao akitanguliwa na kaka yake aitwaye Nassor Fadhir anayeishi jijini Cologne, nchini Ujerumani.

MALENGO YAKE
Mbwiga ambaye anapenda kujitambulisha kuwa ni mzaramo, anasema ana mpango wa kujiendeleza kielimu ili aweze kuitumikia vizuri kazi yake.

“Elimu yangu siyo kubwa sana ila nimesoma pale VETA Chang’ombe kwa miaka miwili na kutunukiwa cheti cha ujenzi wa barabara.

“Baadaye nilijiingiza katika masuala ya ufundi selemala, kwa hiyo, naweza kusema mimi ni fundi selemala mzuri wa fenicha zote za ndani.

“Ili niweze kwenda na wakati, niko katika mikakati ya kujiendeleza kielimu kwa sababu hata wafanyakazi wenzangu wamekuwa wakinihimiza juu ya hilo,” anasema.

Katika mazungumzo yake, anawashukuru wafanyakazi wenzake wote na kuwataja baadhi kwa majina kuwa ni Joseph Kusaga, Ruge Mutahaba, Joyce Shebe, Shafii Dauda, Gerad Hando, Maestro, Alex Luambano, Bonge, PJ na Simalenga.

“Nimewataja hao, lakini lazima umuweke Babra Hassan, yaani usipomtaja huyo, ataninunia mpaka basi,” anatania Mbwiga.
Kajunason Blog

Kajunason Blog

A Tanzanian blog operating since October 2007, covering Local News, Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers / viewers.

Toa Maoni Yako:

0 comments: