RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Alhaj Dk. Amani Abeid Karume amesema kuwa madhumuni makubwa ya jengo jipya la Afisi ya Mufti Mkuu wa Zanzibar ni kuendeleza shughuli za kusimamia umoja na mshikamano wa kidini kwa wananchi wote wa Zanzibar.

Wito huo umetolewa leo na Alhaj Karume mara baada ya kulizindua rasmi jengo jipya la Afisi ya Muftii Mkuu wa Zanzibar lililopo Mazizini mjini Unguja lililojengwa kwa msaada wa Serikali ya Oman kutokana na juhudi binafsi za Sheikh Ahmad Al-khaliyl ambaye ni Mufti Mkuu wa nchi hiyo.

Alhaj Dk. Karume alisema kuwa jengo hilo litasaidia kwa kiasi kikubwa kutoa elimu na taaluma kwa Waumini wa dini ya Kiislamu na kusisitiza kuwa afisi hiyo itumike zaidi kwa kuendeleza mshikamano.

Alhaj Karume alisema kuwa historia ya Zanzibar inaonesha kuwa kutofautiana katika suala la kuandama kwa mwezi mtukufu wa Ramadhani kulikuwepo tokea siku za nyuma kwani madhehebu ya Mabohora yalikuwa yakitofautiana na madhehebu mengine katika muandamo wakuandamisha mwezi huo lakini walizingatia heshima kwa madhehebu mengine.

“Tulikuwa tunatofautiana lakini katika jambo hilo tumejifunza ni kuwa wenzetu walikuwa wakitangulia mapema na wanasali Iddi katika msikiti wao na matayarisho yote yalikuwa yakifanywa kimya kimya na siku ya pili wote tulisherehekea Iddi kwa mashirikiano na hapakutokea ugomvi wala msukumano....hii ni imani tu lakini dini ni ile ile”,alisisitiza Alhaj Karume.

Kutokana na hali hiyo, Rais Karume alisema kuwa hakuna haja ya kugombana miongoni mwa Waislamu na badala yake Afisi ya Mufti inatakiwa kutoa elimu na taaluma kwa Waislamu na wale wote wenye kufuata njia hiyo.

Katika hotuba yake, Alhaj Karume alipongeza kazi nzuri zinazoendelea kufanywa na Afisi ya Mufti ikiwemo kutoa elimu, mawaidha na taaluma na kuitaka afisi hiyo kuendelea kufanya hivyo kwani kuna baadhi ya watu hufanya mambo kwa vile hawaelewi lakini wakipata elimu huelewa. Pia, Dk. Karume alisisitiza kuwa pongezi hizo zichukuliwe na afisi hiyo kama changamoto za kufanya vizuri zaidi.

Aidha, aliitaka Afisi hiyo kusimamia vizuri masuala ya mirathi kwa kuwapa haki zao mayatima,vizuka na watoto wa kike.

Sambamba na hayo, Rais Karume aliitaka afisi hiyo kuendeleza mahusiano na maelewano na dini nyengine hapa nchini na kuitaka Afisi ya Mufti kusimamia hilo na kutosubiri hadi kutokea tatizo, licha ya kuwa historia inaeleza kuwa halijawahi kutokea tatizo lolote la kidini hapa Zanzibar.

Alieleza kuwa mahusiano mazuri ya kidini yapo hapa Zanzibar katika siku za sikukuu hata wakati wa Mwezi mtukufu wa Ramadhani na hayo ndiyo yaliofanya kuendelea kuwepo mshikamano wa kidini hapa nchini na kusisitiza kuwa afisi hiyo iwe ni macho ya kuona hayo yanatekelezwa kwa kuzidisha mashirikiano zaidi.

Rais Karume alitoa shukurani kwa Mufti Mkuu wa Oman kwa kusimamia kupatikana fedha za ujenzi wa jengo la afisi hiyo hatua ambayo ilitokana na muwaliko alioutoa kwa Mufti Mkuu wa Zanzinar kutembelea nchi hiyo na hatimae kujengwa jengo hilo.

Alisema kuwa watu wa Oman wanahistoria kubwa na wananchi wa Zanzibar na kuwa na utamaduni wa kushirikiana, kutembeleana na hata kuishi pamoja na kusifu maelewano hayo yaliopo.

Alitoa shukurani kwa wananchi wa Omani na Mfalme Qaboos kwa mashirikiano na uhusiano na kuwataka waendelee kupata amani.

Mufti Mkuu wa Oman, Sheikh Ahmed Alkhaliyl alisema kuwa uhusiano wa Oman na Zanzibar ni wa kihistoria na kueleza kuwa Zanzibar ni nchi tukufu na chimbuko la elimu ya dini katika ukanda wa nchi za Afrika Mashariki hali ambayo imemvutia zaidi kusaidia ujenzi wa afisi hiyo.

Mufti Mkuu wa Wazanzibar Sheikh Harith bin Khelef Khamis alitoa shukurani kwa Mufti wa Oman na wananchi wake wote na kutaka uhusiano uliopo uzidi kuendelea kwa manufaa ya nchi mbili hizo.

Mapema Katibu Mkuu wa Wizara ya Nchi Afisi ya Rais Katiba na Utawala Bora, Mahadhi Juma alisema kuwa ujenzi wa jengo hilo ulianza Mei 6, mwaka 2006 chini ya Kampuni ya Mazrui Building Contractors ya Zanzibar chini ya ushauri wa Al-Habibi Consultant kutoka Dar-es-Salaam ambao umegharimu jumla ya Riali 65,000 sawa na dola 170,000 za Kimarekani.

Alisema kuwa Serikali kwa upande wake imechangia shilingi milioni 48 ambazo zimetumika kwa ujenzi wa uzio ili kuiweka afisi katika hali ya usalama na inayovutia zaidi.

Katibu Mkuu huyo, alisema kuwa jengo hilo lina sehemu kubwa ya mapokezi, afisi ya walinzi, vyumba viwili vikubwa vya afisi kwa ajili ya Mufti Mkuu na Katibu wa Mufti, chumba cha kusalia kina mama, jiko, ukumbi wa mikutano unaweza kuchukua watu kati ya 35 hadi 45 na afisi 7 za maafisa wa afisi hiyo pamoja na sehemu nyenginezo.

Alieleza kuwa jengo hilo limejengwa katika hali ambayo inaruhusu kuongezwa ghorofa moja juu iwapo mahitaji yatatokea na hali itaruhusu.

Katika uzinduzi huo viongozi mbali mbali wa dini na serikali walihudhuria.


Habari kwa hisani ya Rajab Mkasaba wa Ikulu Zanzibar.
Kajunason Blog

Kajunason Blog

A Tanzanian blog operating since October 2007, covering Local News, Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers / viewers.

Toa Maoni Yako:

0 comments: