WAALIMU wa Zanzibar wameeleza kuwa kuimarika kwa uchumi na maendeleo na kuongoza nchi kwa juhudi, busara na hekima kubwa ni miongoni mwa sababu za kupewa heshima ya Udaktari wa Falsafa ya Sheria Rais Karume.

Aidha, kukubalika kuonesha uwezo mkubwa katika kuleta mshikamano na mashirikiano miongoni mwa wananchi wa Zanzibar na kurejesha imani kwa washirika wa Maendeleo na kupata misaada mbali mbali ya maendeleo ya Taifa pia ni miongoni mwa sababu hizo.

Waalimu hao waliyasema hayo katika risala yao ya kumpongeza Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe. Dk Amani Abeid Karume kwa kutunukiwa Shahada ya Heshima ya Udaktari wa Falsafa ya Sheria katika Chuo Kikuu cha Taifa cha South Carolina nchini Marekani mnamo tarehe 9, Mei mwaka huu.

Sherehe hizo zilifanyika katika viwanja vya Victoria Garden iliopo katika manispaa ya mjini Unguja na kuhudhuriwa na viongozi mbali mbali wakiwemo wakuu wa vyuo vikuu, Wabunge, Wawakilishi, Mabalozi na viongozi na waalimu na wanafunzi wa vyuo vikuu vya Zanzibar pamoja na wananchi mbali mbali.

Katika sherehe hiyo ambayo imeandaliwa na Waalimu wa Zanzibar wakishirikiana na Chuo Kikuu cha Taifa (SUZA) walieleza kuwa katika muda wote wa uongozi wa Rais Karume ameweza kuonesha ukomavu katika kuimarisha demokrasia, utawala bora na haki za binaadamu.

Walieleza kuwa Dk. Karume ameiwezesha nchi ya Zanzibar kuwa katika hali ya amani na utulivu wa kupigiwa mfano, mambo ambayo ni nyezo muhimu katika kuleta ustawi wa jamii.

Walisema kuwa sekta za utoaji huduma nazo zimeimarika, ujenzi wa vituo vya afya umeshamiri na huduma za matibabu zinapatikana kwa kiwango cha kuridhisha ambapo ugonjwa wa Malaria ambao ulikuwa tishio kubwa kwa wananchi wa Zanzibar na nchi nyengine duniani umepungua kwa kiasi kikubwa.

Waalimu hao walisema kuwa hali hiyo imefikiwa kutokana na usimamizi mzuri wa utekelezaji wa mradi wa KATAA MALARIA ulio chini ya ufadhili wa Rais George W. Bush wa Marekani.

“Sekta ya elimu nayo imeimarika sana tangu mwaka 2000, kila mtoto aliyefika umri wa kwenda skuli anapata elimu bila ya malipo, skuli zimeenea ambapo hapana mtoto anayekwenda zaidi ya kilomita 5 kufuatia masomo...zaidi ya hivyo katika kipindi chako umeweza kuanzisha Chuo Kikuu cha Taifa”walieleza waalimu hao.

Aidha, katika risala yao hiyo waalimu hao walieleza kuwa maji safi na salama, maakazi na huduma nyengine za jamii zimeimarika mara dufu katika uongozi wa Rais Karume pamoja na mishahara na mafao ya wafanyakazi wastaafu yanapatikana kwa wakati tafauti na ilivyokuwa hapo kabla.

Pamoja na hayo walieleza kuwa Rais Karume ameweza kuimarisha miundombinu ikiwemo ile ya barabara za lami jambo ambalo limewapunguzia shida wananchi katika kujiletea maendeleo yao.

“Waswahili wanasema, ‘chanda chema huvikwa pete’. Kwa mafanikio hayo tuliyoyataja hapana ambaye angeweza kusema hustahiki shahada uliyotunukiwa”walisisitiza waalimu hao.

Mapema Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Amali Mhe. Haroun Ali Suleiman alifafanua kuwa Udaktari wa Rais Karume umepita ngazi mbali mbali za kitaalamu na kupita katika mikondo mingi ya vigezo vya uwajibikaji tokea utumishi wake akiwa Mwakilishi, Mbunge, Waziri wa Biashara, Waziri wa Mawasiliano na hadi kugombania nafasi ya Urais wa Zanzibar na kuwa Rais.

“Magwiji wamekaana kufanya utafiti wa watu wanaostahiki kupewa heshima hii, ambayo tayari viongozi wakuu wa Marekani wamepata akiwemo aliyekuwa Makamu wa Rais wa Marekani Algore na wengineo wachache’,alisema Haroun.

Nae Rais Karume kwa upande wake aliwataka Wazanzibari wote kutojidharau kwani wana uwezo mkubwa katika shughuli za kujiletea maendeleo na kueleza kuwa heshima hiyo ameipata kutokana na mashirikiano ya wananchi wote wa Zanzibar.

Akihutubia katika sherehe hizo ambazo zilihudhuriwa na mamia ya wananchi Rais Karume alisema kwa kiasi kikubwa anawashukuru wananchi wa Zanzibar kwa kuweza kumpatia kuwa na sifa na kutoa nasaha na maoni kutokana na tunzo hiyo kwamba juhudi za kujenga nchi na kuwaletea maendeleo wananchi zinatizamwa na kuzingatiwa kimataifa. “ Kwa hivyo ni lazima tuwe viongozi na watu wenye bidii, uaminifu, kujitolea kutumikia wananchi, kuchapa kazi na wenye kuona mbele, yaani tuwe na nadhari”,alisema Dk. Karume.

Aidha, Rais Karume alitoa pongezi zake kwa Wawakili na Baraza la Senate la chuo cha South Carolina, Marekani, waliopitisha azimio la kukitaka Chuo hicho kumpa heshima hiyo. Na kueleza kuwa Chuo hicho kimeahidi kuendelea kuisaidia Zanzibar katika kukuza mafunzo ya ualimu,kutoa nafasi za masomo katika chuo hicho,kubadilishana waalimu, kutembeleana sambamba na kuendelea na mpango wa kuchapishwa vitabu mpaka kufikia vitabu vya shule za msingi.

Habari kwa hisani ya Rajab Mkasaba wa Ikulu Zanzibar.
Kajunason Blog

Kajunason Blog

A Tanzanian blog operating since October 2007, covering Local News, Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers / viewers.

Toa Maoni Yako:

0 comments: